Mwanafunzi aliyeokota bomu la kutupa kwa
mkono akidhani ni chuma chakavu kwa lengo la kwenda kuuza imebainika
kuwa ni miongoni mwa watano waliokufa baada ya kulipuka na kujeruhi
wengine 43, akiwemo mwalimu wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustino Ollomi amemtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Juliana Tarasisi (13).
Amesema hayo leo Alhamisi Novemba 9,2017
kuwa, mwanafunzi huyo alilitunza bomu hilo kwenye begi lake la
madaftari ili kwenda kuliuza kwa mnunuzi wa chuma chakavu wakati wa
mapumziko.
Wanafunzi wengine waliopoteza maisha
katika tukio hilo lililotokea jana, Jumatano Novemba 8,2017 ni Evart
Theonas (12) Edson Bigilimana (12), Miburo Gabriel (12), na Tumsifu
Ruvugo (8).
Wanafunzi 42 wa darasa la kwanza katika
Shule ya Msingi Kihinga na mwalimu wao wa darasa, Policalipo Clemency
aliyekuwa darasani wakati wa tukio wamelazwa kwa matibabu katika
Hospitali ya Misheni ya Rulenge.