Kutoka Dodoma: Serikali yaomba saa 24 kutekeleza agizo la Spika Ndugai

SERIKALI imeomba saa 24 zaidi kutekeleza agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoa taarifa kamili kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kikwazo cha kutakiwa kulipa fedha za usajili wanaporipoti vyuoni.

Juzi, Spika Ndugai aliipa serikali saa 24 kuhakikisha inatoa taarifa kamili bungeni kuhusu kadhia hiyo ambayo alisema imekuwa tatizo la kitaifa.

Kwa mujibu wa Spika Ndugai, taarifa ya serikali kuhusu suala hilo ilipaswa kutolewa jana asubuhi mara tu baada ya kipindi cha 'Maswali' kumalizika.

Hata hivyo, baada ya Mwenyekiti wa Bunge Mussa Zungu, aliyekuwa anaongoza kikao cha jana, kuipa fursa serikali kuwasilisha taarifa yake bungeni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, alikiomba Kiti cha Spika kutoa nafasi nyingine ya siku moja kwa serikali kuandaa taarifa hiyo.

Waziri huyo alisema taarifa hiyo itawasilishwa bungeni leo ikizingatia maslahi mapana ya taifa.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maslahi mapana ya wananchi na wanafunzi wa elimu ya juu, naomba kauli ya serikali iwasilishwe kesho (leo)," Prof. Ndalichako alisema na kumuomba Zungu aridhie ombi hilo la serikali.

Zungu aliridhia ombi hilo na kuitaka serikali kutekeleza agizo la Spika Ndugai leo.

Spika Ndugai alitoa agizo hilo juzi bungeni mjini hapa alipokuwa akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM).

Mara tu baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali', mbunge huyo alisimama na kutumia Kanuni ya 68(7) kuomba mwongozo wa Spika kuhusu kadhia za aina tatu wanazokumbana nazo wanafunzi wanaoporipoti vyuoni kuanza masomo.

Alisema jambo la kwanza ni wanafunzi wengi waliofaulu kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu wamekosa nafasi ilhali wana sifa ingawa alikiri pia idadi ya waliopata nafasi hiyo ni kubwa.

"La pili, katika wale waliopata nafasi za kuingia vyuo vikuu, wengine wanastahili kupata mkopo lakini wengi pia hawakupata mkopo," alisema.

"Jambo la tatu ni kwamba, pamoja na kuwa kuna wanafunzi ambao wamepata mkopo, bado kuna tatizo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais alishalitolea maelekezo -- wanafunzi hawa waliopata mkopo wanapofika vyuoni wasisumbuliwe, wapokelewe ili waanze masomo yao."

Alisema kumekuwa na tatizo wananfunzi wakifika vyuoni wanatakiwa walipe fedha ya kusajiliwa na chuo.

"Tatizo hili ni kubwa. Wanafunzi wengi wako nje na sisi wabunge tumeombwa sana na wanafunzi hawa ili tuwalipie fedha za kusajiliwa ili wawe wanafunzi pamoja na kwamba wana mkopo," alisema.

"Sasa katika mambo haya matatu, Mheshimiwa Spika naomba mwongozo wako ili serikali iseme ni kitu gani ambacho inaweza ikafanya ili kuondoa tatizo hili."

Katika mwongozo wake, Spika Ndugai alisema: "Jambo hili ni 'serious' kabisa, ni 'serious' kabisa! Wala si wa mwaka wa kwanza peke yake, na wa miaka mingine, awe wa mwaka wa pili, mwaka wa tatu.

"Yaani mtu ana mkopo, anatakiwa akifika chuoni, alipe kwanza fedha za kuwa 'registered' (kusajiliwa) pale chuo halafu sasa akishasajiliwa na chuo ndipo sasa aandikishwe apate haki yake ya mkopo.

"Sasa, waheshimiwa hawa ni watoto wa maskini, kwa hiyo wanazagaa nchi nzima ni matatizo makubwa.

"Kwa hiyo tunaomba kesho (jana) baada ya tu ya maswali (kipindi cha 'Maswali' bungeni), serikali itoe tamko au taarifa kamili ya kuhusu nini kinachoendelea kuhusu hili jambo la mtu ana haki yake, hapewi mpaka pale utaratibu ambao unatakiwa hela.

"Na ndiyo maana alipata mkopo kwa sababu hana kitu, halafu anatakiwa atoe hela apate haki yake. Sasa, kesho serikali ituambie lipi ni lipi katika jambo hili."

Nipashe ilifuatilia kwenye tovuti rasmi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na kubaini kuwa kwa mwanafunzi anayejiunga na kitivo cha Sayansi ya Afya cha chuo hicho kuchukua shahada ya kwanza, stashaha na astashahada, kwa mfano, anatakiwa kulipa Sh. 300,250 au Dola za Marekani 250 (kwa wanafunzi wa kigeni) zikiwa ni gharama zinazolipwa moja kwa moja (direct costs).

Pia anatakiwa kulipa Sh. 10,000 kwa ajili ya umoja wa wanafunzi, bima ya afya (NHIF) Sh. 50,400 au NSSF Sh. 60,000 (Akiba Afya Plus) na Sh. 20,000  kwa ajili ya ithibati (Quality Assurance Fee).

Nipashe pia ilipitia tovuti rasmi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) juzi na kubaini kuwa mwanafunzi anatakiwa kulipa Sh. 97,400 kila mwaka wa masomo kwa ajili ya gharama za moja kwa moja (direct costs).